News Details

Event

Vyuo Vikuu Tanzania Vyatakiwa Kuchangamkia Fursa Nchini Malawi

21 Sep Joseph Kiphizi Wed 21 Sep 2022

Balozi wa Tanzania nchini Malawi Mhe.Humphrey Polepole amevitaka vyuo vikuu nchini Tanzania kuchangamkia fursa lukuki zinazopatikana nchini Malawi hususani katika maeneo ya tafiti, kubadilishana wanafunzi na kufundisha lugha ya Kiswahili hasa wakati huu ambapo Malawi imeanzisha somo hilo kwa shule za msingi na sekondari.

Mhe.Polepole ametoa rai hiyo katika ziara aliyoifanya Chuo Kikuu Mzumbe, Kampasi Kuu Morogoro na kuzungumza na Menejimenti ya chuo hicho ambapo alikipongeza kwa utendaji wake wa kuzalisha Wanataaluma nguli kwa miaka mingi na kuahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha kinapenya nchini Malawi na kuanzisha mashirikiano ya kimkakati na vyuo vikuu vilivyopo nchini humo.

“Vyuo vikongwe vina jukumu la kulea vyuo vidogo,nanyi Chuo Kikuu Mzumbe ni moja kati ya vyuo vikubwa  na wabobezi katika masuala ya Menejimenti na utawala kwa umma.Viongozi wengi wa Afrika walipita hapa, njooni Malawi muwajengee uwezo katika masuala ya tafiti na utawala bora.” Alisisitiza

Awali akimkaribisha Balozi, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof.William Mwegoha alimweleza kuwa, chuo kimeendelea kufanya vizuri kwenye majukumu yake ya msingi na kwamba kutakuwa na mabadiliko makubwa zaidi hivi karibuni kupitia mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) utakaojenga miundombinu mipya na kufanya maboresho ya mitaala na hivyo kumshukuru kwa kutambua nafasi ya chuo kikuu Mzumbe katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya Malawi na Tanzania

Nae Rasi wa Ndaki ya Mbeya ya Chuo Kikuu Mzumbe Prof.Henry Mollel, alimshukuru Balozi Polepole kwa kuwasilisha fursa zilizopo nchini Malawi na kusema kuwa hatua hiyo imeongeza uelewa wa kutambua fursa nyingi zaidi ya zile walizokuwa wakiziona na kwamba inatoa msukumo na ari kubwa kwa Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Mbeya kuendelea na mchakato wa kuunda mashirikiano ya kimkakati waliokuwa wameuanzisha baina yao na Chuo Kikuu cha Malawi kwa kushirikiana kwa karibu zaidi na Balozi.

0 Comments

No Comments at the moment