News Details

Event

Maandalizi Ya Hafla Ya Kumkabidhi Mshauri Mwelekezi Eneo La Kujenga Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki Ya Tanga Yakamilika

17 Jan Joseph Kiphizi Wed 17 Jan 2024

Chuo Kikuu Mzumbe ambacho kwa sasa kina ndaki mbili (Ndaki ya Dar es salaam na Mbeya) kipo katika maandalizi ya kuanzisha ndaki ya tatu jijini Tanga.

Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi, "Higher Education for Economic Transformation - HEET Project," kimeandaa hafla ya kukabidhi eneo la ujenzi wa Ndaki Tanga kwa Mshauri Mwelekezi tayari kwa kuanza usanifu wa miundombinu. Hafla hiyo inatarajiwa kufanyika tarehe 08 Januari 2024.

Maandalizi ya hafla hiyo yamefanywa na wawakilishi wa Chuo Kikuu Mzumbe wakiongozwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko Bi. Lulu Mussa pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Mkinga Mhe. Kanali Hassan Maulid Surumbu, walipokutana tarehe 05 Januari 2024 katika makao makuu ya Wilaya hiyo.

Mkuu wa Wilaya amesema Chuo Kikuu Mzumbe kimeonesha dhamira ya dhati katika kutoa mchango wa maendeleo ya elimu na uchumi nchini Tanzania. Aidha, imedhihirika wazi kwamba Ndaki hiyo itapokamilika, itachochea wigo mpana wa kutoa huduma za kitaaluma (utafiti, ushauri wa kitaaluma, huduma za kijamii) na hatimaye kuleta maendeleo siyo tu nchini Tanzania bali pia katika eneo la Afrika Mashariki kwa ujumla.

Kukamilika kwa ujenzi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Tanga utakuwa ni upanuzi mkubwa wa Chuo hicho, hali itakayoendana na kupanua huduma tajwa zinazotolewa na Chuo Kikuu Mzumbe. Huu utakuwa utekelezaji thabibiti kaulimbiu ya Chuo Kikuu Mzumbe: Tujifunze kwa maendeleo ya watu.

Mhe.Kanali Hassan Maulid Surumbu ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo imewezesha kufikiwa na Mradi wa HEET ambao umekuwa msaada mkubwa katika kutekeleza mpango wa kujenga Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Tanga.

1 Comments

Kyejoaugustino22@Gmail.Com - Wed 07 Feb 2024 13:16 p.m.
big up my blessed university MZUMBE AKA MILITARY UNIVERSITY