News Details

Event

Dk. Kijaji Awataka Wanafunzi Vyuo Vikuu Kurejesha Uzalendo

26 Nov Joseph Kiphizi Fri 26 Nov 2021

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dk Ashatu Kijaji amewataka wanafunzi wa vyuo vikuu nchini kurejea kwenye uzalendo, miiko na maadili mema ya Kitanzania yatakayowaongoza kwenye mafanikio.

Dk Kijaji ameyasema hayo leo Jumatano Novemba 24, 2021, wakati wa mkutano wa baraza la wahitimu wa Chuo Kikuu Mzumbe cha mkoani Morogoro.

Amesema mafaniko yoyote ikiwemo suala la uongozi lazima kutanguliza mbele uzalendo na kuonyesha mfano kwa watu unaowaongoza, hivyo amewataka vijana katika chuo cha Mzumbe kuwa mfano wa kuigwa wanapokuwa chuoni na wanapomaliza masomo yao.

“Bado kuna wazazi na watu wengi wana mtazamo hasi kwa watoto wao wakifika hatua ya kwenda chuo, wanawaza huko kuna mambo mabaya hadi kufikia wazazi wengine kuwazuia watoto wao, sasa niwaeleze mimi nimesoma hapa Mzumbe nikapata mume nikiwa chuoni, nilijua kilichonileta nikamuwekea mtazamo wangu mume akanielewa na tukamaliza wote chuo mpaka sasa tunaendelea vyema,”alisema.

Amesema Mtazamo huo hasi unaweza kuondolewa na wanafunzi wenyewe hususani wanafunzi kike kwa kujikita katika uzalendo na maadili ya Kitanzania.

Dk Ashatu amesema viongozi wengi wanaofanya kazi nzuri hapa nchini wengi ni zao la Mzumbe ambao ni tegemeo la Taifa.

Amesema “Rais  Samia  Suluhu Hassan ni miongoni mwa zao la  Mzumbe na amekuwa mfano wa kuigwa amefanya mambo makubwa tangu aingie madarakani kama Mzumbe tunatakiwa kujivunia hilo na tunaona mambo mazuri yanayofanyika,”.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Jamal Kassim Ali amesema ili mtu yoyote aweze kufanikiwa ni lazima awe na malengo na kujiamini sambamba na kufanya maamuzi magumu pale anapoona inabidi.

Ametoa wito kwa vijana kuwa pamoja na ndoto walizonazo katika maisha lazima wazifunganishe katika tija kwa kuangalia maslahi ya taifa kwanza.

Makamu mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Lugano Kusiluka amesisitiza umuhimu wa kupata maoni ya wahitimu mbalimbali waliopo kwenye mamlaka hali itakayoibua mafanikio ya chuo na wanafunzi kwa ujumla.

0 Comments

No Comments at the moment